Miaka 10 jela kwa kudhihaki ufalme Thailand

Imebadilishwa: 23 Januari, 2013 - Saa 11:45 GMT

Mwanaharakati Somyot Pruksakasemsuk,awasili mahakamani Bangkok

Mahakama nchini Thailand imemuhukumu mhariri wa jarida moja miaka kumi gerezani kwa kuchapisha taarifa zinazoaminika kuudhihaki ufalme.

Somyot Pruksakasemsuk, ambaye pia ni mwanaharakati mashuhuri wa kisiasa alipatikana na hatia ya kuchapisha nakala mbili zilizokwenda kinyume na sheria kali za kulinda ufalme wa nchi hiyo.

Alizuiliwa bila dhamana tangu Aprili mwaka wa 2011 na wafuasi wake wameteta mara kadhaa kuwa aliteswa kizuizini.

Alihukumiwa chini ya sheria ya Thailnd kuhusu ufalme, ambayo wanhaarakati wanasema inatumika kuhujumu uhuru wa kujieleza.

Mashirika ya kutetea haki za kibindamu pamoja na Muungano wa Ulaya wamekashifu vikali hukumu hiyo.

Muungano wa bara Ulaya unasema hukumu hiyo inahujumu uhuru wa kujieleza pamoja na uhuru wa vyombo vya habari.

''Wakati huohuo, inachafua sifa ya Thailand kama nchi huru na yenye demokrasia,'' alisema mjumbe wa Muungano huo.

Jarida la Somyot linahusishwa na vuguvugu la "red-shirt" lililoongoza maandamano dhidi ya serikali mwaka 2010 yaliyosababisha kufungwa kwa baadhi ya maeneo ya Bangkok.

Alikuwa amezuiliwa bila dhamana tangu mwezi Aprili mwaka 2011 na wafuasi wake wamelalamika kuwa aliteswa wakati akizuiliwa.

Nakala hizo mbili zilizomletea masaibu yake mwandishi huyu, zilichapishwa mwaka 2010 chini ya majina bandia kwenye jarida hilo alilolianzisha.

Somyot alikamatwa mwaka mmoja baadaye baada ya kutoa ombi la kufanyia mageuzi kipengee cha 112 ambacho kinasema kuwa yeyote atakayeutusi ufalme kwa lolote, atafungwa jela.

Mahakama ilimhukumu miaka mitano kwa kila taarifa aliyoichapisha na kuongezwa mwaka mmoja kwa sababu ya kesi moja iliyomhusu kuhusiana na swala lilo hilo na ambayo iliakhirishwa kusikilizwa miaka mitatu iliyopita.

Wakili wake amesema atakata rufaa dhidi ya hukumu hiyo.

Wengi nchini Thailand wameelezea kushangazwa na adhabu hiyo wanayosema ni kali mno.

Sheria ya ufalme ya Thailand, inanuia kuulinda ufalme huo unaoongozwa na mfalme Bhumibol Adulyadej, mwenye umri wa miaka 85 lakini wakosoaji wanasema kuwa ufalme huo umejihusisha sana kisiasa.

Taarifa zinazohusiana

BBC © 2014 Ilani: BBC haihusiki na yaliyoandikwa na tovuti za nje ya BBC.

Ukurasa huu unaonekana vyema kwa kivinjari cha kisasa kikiwa na laha mtindo (CSS).Wakati unaweza kuona yaliyomo katika ukurasa huu kwa kivinjari ulichonacho, hautaweza kufaidi kuona kila kitu vizuri. Tafadhali zingatia uwezekano wa kuboresha progaramu ya kivinjari au kuwezesha laha mtindo (CSS) endapo unaweza kufanya hivyo.