Mshambulizi amlenga waziri mkuu Somalia

Image caption Wanajeshi walimzuia kuingia katika ofisi ya waziri mkuu

Mtu mmoja ameuawa na wengine kujeruhiwa katika shambulizi la kujitoa mhanga nchini Somalia ambapo mshambuliaji amejilipua karibu na ofisi za waziri mkuu

Mlinzi mmoja aliyeshuhudia shambulio hilo alisema kuwa polisi mmoja aliuawa na wengine wawili kujeruhiwa.

Lakini kwa mujibu wa maafisa wa utawala, watu wawili wameuawa na wengine wengi kujeruhiwa katika shambulio hilo lililotokea karibu na makao ya Rais mjni Mogadishu.

Mwandishi wa BBC Abdullahi Sheikh mjini Nairobi anasema kuwa maafisa wakuu wanaelezea kuwa lengo la mshambuliaji lilikuwa kulipua ofisi ya waziri mkuu Abdi Farah Shirdon.

Lakini wanajeshi waliokuwa wanashika doria walisema walimzuia kufika katika ofisi hiyo.

Aidha maafisa walidokeza kwamba mshambuliaji alijilipua alipokuwa anahojiwa katika kizuizi kimoja cha polisi karibu na ofisi hiyo.

Mshambuliaji alijilipua karibu na ukuta unaotenganisha ubalozi wa Ethiopia na makao ya waziri mkuu.

Majengo hayo mawili yako ndani ya eneo ambalo pia linahifadhi makaazi ya rais.

Idadi ya washambuliaji wa kujitoa mhanga imekuwa ikipungua tangu wanamgambo wa Al Shabaab kuondoka Mogadishu kuanzia Agosti 2011 lakini hili li dhihirsiho la changamoto inayowakabili maafisa wa usalama katika kupambana na wanamgambo hao.