Miezi 18 katika chumba cha kuhifadhia maiti

Image caption Fortune Adzawoloo, alifariki mwaka 2011

Mwili wa raia wa Ghana aliyekuwa anafanya kazi ya uvuvi Ireland Kaskazini , bado uko kwenye chumba cha kuhifadhia maiti, zaidi ya mwaka mmoja baada ya kifo chake.

Juhudi za kutaka kuurejesha mwili wake nyumbani kwao mazishi hadi kufikia sasa hazijafanikiwa.

Fortune Adzawoloo, 29, alifariki mwezi Julai mwaka 2011, wiki sita baada ya kuanza kazi yake ya uvuvi.

Familia yake, inataka mwili wake kurejeshwa nyumbani lakini wanazozana kuhusu nani atagharamia safari hiyo.

Bwana Adzawoloo alipelekwa hospitalini tarehe 18 mwezi Julai mwaka 2011, lakini akafariki baadaye siku hiyo.

Mwili wake baadaye ulipelekwa katika hospitali ya Royal Victoria mjini Belfast ambako bado unasalia kuwa katika chumba cha kuhifadhia maiti.

Shirika moja limejotolea kulipia mazishi yake lakini sharti yafanyike nchini humo lakini jamaa zake wamekataa pendekezo hilo.

Kulingana na mwakili wa kisheria wa familia hiyo, marehemu alikuwa chifu katika jamii yake nchini Ghana.

Tamaduni za watu wa Ghana zinasema kuwa anapaswa kuzikwa mahala maalum nyumbani kwao.