Wauawa kwa kutoa chanjo ya Polio Pakistan

Image caption Watu 12 tayari wameuawa nchini Pakistan kwa sababu ya kutoa chanjo ya Polio

Maafisa nchini Pakistan wanasema kuwa maafisa wawili wa afya waliokuwa njiani kwenda kutoa chanjo dhidi ya ugonjwa wa Polio, wameuawa katika shambulio la bomu lililokuwa limetegwa kando ya barabara.

Shambulizi hilo limetokea katika eneo la kikabila Kaskazini Magharabi mwa nchi.

Afisaa wa serikali alisema kuwa wafanyakazi hao waliokuwa wanaelekea kijijini kutoa chanjo kwa watoto, waliuawa wakati bomu lilipolipuka.

Shambulizi la leo linafikisha idadi ya wale waliouawa mwezi jana kwa sababu ya kutoa chanjo ya Polio hadi watu 12.

Wapiganaji wa Taleban, wamekuwa wakilaumiwa kwa kutekeleza mashambulizi hayo.

Kundi hilo la wanamgambo, limeharamisha chanjo kwa watoto wakisema kuwa ni njama ya Marekani kufanya ujasusi nchini humo pamoja na kuwa chanjo hiyo inawaondolea watoto uwezo wa kuzaa.