Serikali ya Zimbabwe yafilisika?

Image caption Waziri wa Fedha Tendai Biti

Waziri wa Fedha wa Zimbabwe Tendai Biti amesema kwamba wiki iliyopita nchi hiyo ilifika mahali ambapo ilibaki na dola 217 tu katika akaunti yake ya umma, baada ya kuwalipa wafanyikazi wa serikali.

Hata hivyo alisema kwamba dola milioni 30 za mapato ziliingia siku iliyofuata.

Bwana Biti aliiambia BBC kuwa alifichua haya ili kusisitiza kwamba serikali ilikuwa haina fedha za kugharamia uchaguzi, lakini siyo kwamba ilikuwa imefilisika.

Uchaguzi mkuu umepangwa kufanywa mwaka huu, ambapo chama cha Rais Mugabe cha Zanu-PF kitapingana na cha Bwana Biti cha Movement for Democratic Change.

Awali, Bwana Biti alikuwa amelalamika kwamba makampuni yanayochimbua almasi yalikuwa hayawasilishi mapato yao kwa serikali.

Serikali ya muungano

Serikali ya muungano iliyoundwa mnamo 2009 imeweza kukomesha miaka mingi ya mfumko mkali wa bei kwa kuamua kwamba sarafu ya kutumika ingekuwa ni dola ya Marekani. Hata hivyo uchumi wa nchi hiyo haujajengekeka vilivyo.

Bwana Biti alikiambia kipindi cha redio cha BBC cha Focus on Africa kwamba matamshi yake yalikuwa yameeleweka visivyo, na kwamba wanahabari walifanya hivyo makusudi.

"Nyie waandishi mu wachokozi sana, na nia zenyu mbaya. Nilichokuwa nasema mimi ni kwamba serikali ya Zimbabwe haina fedha za kugharamia uchaguzi au kura ya maoni," he said.

Zimbabwe inahitaji takriban dola milioni 200 ili kugharamia kura ya maoni kuhusu katiba mpya, na kufanya uchaguzi.