25 wauawa kwenye mlipuko Mexico

Idadi ya watu waliouawa katika mlipuko uliotokea katika mji mkuu wa Mexico, Mexico City kwenye makao makuu ya kampuni ya tiafa ya mafuta, Pemex, imeongezeka na kufikia watu 25.

Hii ni kwa mujibu wa waziri wa mambo ya ndani wa nchi hiyo .

Takriban watu 100 walijeruhiwa na wengine ambao idadi yao haijulikani wakinaswa chini ya vifusi katika jengo lenye ghorofa 54. Shughuli ya kuwatafuta manusura ingali inaendelea.

Chanzo cha mlipuko huo bado hakijulikani kwani uchunguzi ungali unaendelea.

Septemba mwaka jana, watu 30 waliuawa kwenye mlipuko katika kiwanda cha gesi Kaskazini mwa Mexico.

Wasiwasi wa jamaa

Mlipuko huo uliotokea Alhamisi katika sehemu za chini za jengo hilo,ulitokea wakati watu wakibadilishana zamu nyakati za mchana.

Picha za televisheni zilionyesha vifusi kutoka kwenye mlipuko vikisambaa kwenye barabara za mji mbele ya jengo hilo huku msaada wa dharura ukitolewa kwa majeruhi.

Mamia ya waokoaji wakisaidiwa na mbwa maalum wangali wanawatafuta manusura zaidi ya thelathini ambao inaaminika wamenaswa ndani ya jengo hilo.

Polisi wameweka vizuizi katika sehemu ambapo mlipuko huo ulitokea, na ambalo liko katika sehemu yenye shughuli nyingi.

Image caption Polisi wangali wanawatafuta manusura

Jamaa za wafanyakazi waa kampuni hiyo, wamekusanyika nje ya jengo wakiwatafuta jamaa zao au kutaka kupata habarikuhusiana na jamaaa zao.

Kampuni ya Pemex, imesema shughuli zake zitaendelea kama kawaida, na kwamba huduma zote za kifedha na zitaendelea kutolewa.

Mkurugenzi mkuu wa kampuni hiyo Emilio Lozoya Austin, alilazimika kusitisha safari yake ya kuelekea barani Asia baada ya mlipuko huo kutokea.