Upinzani waitisha maandamano zaidi Misri

Image caption Viongozi wa upinzani

Wapinzani wa rais wa Misri wameitisha maandamano zaidi , wiki moja baada ya ghasia ambazo zilisababisha mauaji mengi zaidi tangu rais Morsi achukue mamlaka mwaka jana.

Zaidi ya watu sitini wameuawa . Jana wanasiasa waliafikiana kwa kauli moja kulaani ghasia na kufanya mazungumzo kama njia ya kumaliza mzozo unaoikumba nchi hiyo.

Viongozi hasimu wametangaza kuwa na matumaini baada ya kuwa na mkutano katika chuo kikuu cha Al-Azhar mjini Cairo kikiwa ni chuo cha masomo ya juu kabisa cha taasisi ya waislam wa madhehebu ya Sunni .

Lakini mazungumzo yao yalikaribia kukatizwa pale makundi ya vijana yalipotoa wito wa kufanyika kwa maandamano zaidi dhidi ya rais Mohamed Mosri baada ya sala ya ijumaa.

Walimshutumu kiongozi huyo wa kiislam kwa kulazimisha mageuzi mapya ya kiimla na kukiuka malengo ya mapinduzi yao ya miaka miwili iliyopita .

Kuna mipango ya waandamanaji kukusanyika katika medani ya Tahrir ambapo wanatazamiwa kuandamana hadi kwenye makao ya Rais.

Wafuasi wa bwana Morsi wanasema ni njama ya kutumia nguvu ya maandamano ya mtaani kuuangusha utawala wa kwanza uliochaguliwa wa kidemokrasia nchini Misri