Auawa kwa kuwa mchawi Papua New Guinea.

Mwanamke mmoja aliyedaiwa kuwa mchawi ameuawa kinyama mbele ya umati mkubwa wa watu, katika mojawapo ya miji mikubwa nchini, Papua New Guinea.

Mwanamke huyo mwenye umri wa miaka 20, aliteswa na kuchomwa kwa chuma moto, kumwagiwa mafuta na kisha kuteketezwa juu ya taka katika eneo la Mount Hagen.

Duru zinasema kuwa aliuawa na jamaa za kijana mmoja mdogo aliyefariki hospitalini mapema wiki hii.

Walimtuhumu ,mwanamke huyo kwa kutumia uchawi, kumuua mtoto huyo.

Polisi walijaribu kumwokoa lakini wakafukuzwa na umati uliokuwa umejawa na ghadhabu.

Imani za kishirikina zimeenea kote katika nchi hiyo iliyoko bahari ya Pacific.