Mazishi ya mwanasiasa aliyeuawa Tunisia

Image caption Maandamano yaliyozuka kufuatia mauaji ya mwanasiasa wa upinzani Shokri Belaid

Tunisia inakabiliwa na tisho la mgomo wa kitaifa na hofu ya ghasia zaidi wakati maizshi ya mwanasiasa wa upinzani aliyeuawa siku mbili zilizopita,Chokri Belaid yakifanyika baadaye leo.

Makabiliano yalizuka siku ya Alhamisi kati ya polisi na waandamanaji, mjini Tunis na katika miji mingine.

Waandamanaji waliitaka serikali inayoongozwa na chama tawala cha Ennahda kinachofuata misingi ya dini ya kiisilamu kujiuzulu. Wameilaumu kwa mauaji ya mwansiasa huyo.

Wakati huohuo, chama kinachotawala cha maongozi ya Uislamu cha Ennahda nchini Tunisia kimefutilia mbali pendekezo la Waziri Mkuu la kutaka kuvunjilia mbali Serikali, kufuatia mauaji ya kiongozi wa upinzani.

Vyama vya wafanyakazi vimeitisha mgomo kote nchini humo hii leo, utakaoenda sambamba na mazishi ya kiongozi wa upinzani aliyeuliwa na watu wasiojulikana.

Belaid, alikuwa mkosoaji mkuu wa serikali ya Ennahda.

Hiyo jana kulikuwa na ghasia nyingi katika mji mkuu wa Tunis na katika sehemu zingine nchini ambapo waandamanaji walipambana na polisi.

Waandamanaji wamekuwa wakiitisha kuondoka mamlakani kwa Serikali inayoongozwa na chama cha Ennahda, ambacho wanakilaumu kwa mauaji ya Belaid.

Mwandishi wa BBC mjini Tunis anasema kuwa taifa hilo limegawanyika vikali kati ya kundi linalopendelea mabadiliko, ambalo lilitarajia kupata Serikali ya kidemokrasia kufuatia mapinduzi ya mwaka jana na lile na Waislamu wenye itikadi kali waliopendelea mabadiliko yo yote.