Makampuni yafaa kulipa kodi inayostahiki

Shirika la msaada la Action Aid limetoa wito kwa viongozi wa mataifa tajiri ya G8 watapokutana mwezi Juni, wachukue hatua madhubuti kuzidisha nguvu za sheria za kimataifa kuhusu kodi zinazolipwa na makampuni.

Katika ripoti iliyotolewa Jumapili, Action Aid inadai kuwa Zambia inapunjwa katika kodi inayolipwa na kampuni kubwa ya chakula ya kimataifa - Associated British Foods - kodi ambayo ingeweza kusomesha watoto 48,000 wa Zambia kila mwaka.

Kampuni hiyo haikuvunja sheria, lakini sheria ndivo zilivo hivi sasa.

Uingereza imeshasema kuwa swala lilozusha mjadala mkubwa wa kisiasa la kodi inayolipwa na makampuni ya kimataifa litakuwa katika ajenda ya G8 mwaka huu.

Uingereza ndio rais wa G8 sasa.

Na kampeni hiyo sasa imesisitizwa katika ripoti ya shirika la msaada la Action Aid ambayo inasema makampuni yanafaa kuanza kulipa kodi ya faida inayostahiki katika nchi yanakofanya biashara zao.

Ripoti inakiri kuwa kampuni ya Associated British Foods, ABF, haijavunja sheria na wala siyo peke yake inayofanya hayo.

Lakini Action Aid inatoa hoja kuwa katika miaka mitano iliyopita kibarua katika shamba la ABF nchini Zambia amelipa kodi zaidi kushinda hiyo kampuni ambayo inanufaika na nguvu zake.

ABF imejibu kwamba Zambia imelainisha kodi kwa makampuni na kwamba tangu mwaka wa 2008 kampuni hiyo imewekeza pauni 150-milioni, imejenga kinu kikubwa kabisa cha sukari barani Afrika, imewapatia kazi watu zaidi ya 5,000 na inagharimia miradi ya elimu na afya.