Arejeshwa Uingereza kwa kukiuka sheria Uganda

Uganda imemrejesha nchini Uingereza mtunzi wa mchezo wa kuigiza kuhusu wapenzi wa jinsia moja ambao ulimeletea masaibu hata akakamatwa na kushtakiwa na polisi.

David Cecil alikamatwa kwanza mnamo mwezi Septemba kwa kuonyesha mchezo huo wa kuigiza bila ya idhini kutoka serikali ya Uganda.

Hata hivyo mashtaka dhidi yake yalitupiliwa mbali na mahakama kwa kukosa ushahidi wa kutosha.

Alikamatwa kwa mara nyingine wiki jana huku serikali ikiandaa mipango ya kumrejesha Uingereza, kwa misingi ya kuwa mtovu wa nidhamu.

Cecil ambaye ana famiia Uganda alikamatwa tena wiki iliyopita na kurudishwa Uingereza baada ya serikali ya Uganda kumtaja kuwa mtu asiyetakiwa nchini humo.

Mchezo huo kwa jina "The River and the Mountain, unahadithia mfanyabiashara mmoja aliye katika uhusiano wa wapenzi wa jinsia moja, na aliyeuawa na wafanyakazi wake. Uliigizwa na raia wa Uganda.

Uhusiano wa wapenzi wa jinsia moja ni haramu nchini Uganda.

Cecil, ambaye mpenzi wake ni raia wa Uganda, ambaye wana watoto wawili naye, alikamatwa na maafisa wa uhamiaji Jumatano wiki jana.

Afisaa katika ubalozi wa Uingereza aliambia BBC kuwa Cecil alirejeshwa kwao Jumatatu jioni na kwamba wana wasiwai alirejeshwa bila ya kupewa fursa ya kupinga hatua ya serikali.

Mwezi jana mahakama ilitupilia mbali kesi hiyo baada ya kusema kuwa hakuna ushahidi wa kutosha.

Watu wanaoshiriki mapenzi ya jinsia moja, wamekuwa wakishambuliwa Uganda.

Mwaka jana mwanaharakati David Kato, alipigwa hadi kufariki lakini polisi walikana kuwa mauaji yake yalihusishwa naswala la wapenzi wa jinsia moja.

Bunge la Uganda, linatafakari kuweka sheria itakayoongeza adhabu kwa watakaopatikana na hatia kujihusisha na mapenzi ya jinsia moja.