Mauaji wakati wa maandamano Bahrain

Mvulana mmoja amepigwa risasi na kuuawa nchini Bahrain kwa mujibu wa upinzani Al-Wefaq, aliuawa katika maandamano ya kuadhimisha mwaka wa pili tangu kuzuka mapinduzi katika ufalme wa nchi hiyo.

Kifo cha mvulana huyo ni ukumbusho kwamba mgawanyiko mkali unasalia Bahrain.

Katika ufalme wa nchi hiyo unaoongozwa na madhehebu ya Sunni, idadi kubwa ya madhehebu ya Shia bado yanataka usemi zaidi katika jimbo la Ghuba ambako wanasema wanabaguliwa.

Lakini hivi karibuni mazungumzo yaliyofufuliwa ya kutatua machafuko yanayoshuhudiwa yamekabiliwa na vikwazo.

Waandamanji wanaoipinga serikali hii leo wameweka vizuizi na kukabiliana na vikosi vya usalama, huku wengine wakiimba kupinga mazungumzo ya kitaifa.

Baadhi ya makundi ya upinzani yametaka kufanyike mgomo kuadhimisha siku hii , na yanawashawishi watu wasiende madukani kununua vitu kununua petroli kwenye magari yao au kutumia fedha kwa njia yoyote.