Tarehe ya kura ya maoni Zimbabwe

Mabango ya uchaguzi uliopita
Image caption Mabango ya uchaguzi uliopita

‘Inawezekana’ kwamba kura ya maoni kuhusu katiba mpya ya Zimbabwe itafanyika tarehe 16 Machi. Hivi ndivyo alivyosema waziri wa maswala ya kikatiba, Eric Matinenga.

"Ninaweza kuthibitisha kwamba Machi 16 ndiyo tarehe ‘iliyopendekezwa’," Bwana Matinenga alisema.

"Inabidi mipango ifanywe vizuri ili tuwe na angalau siku mbili za kupiga kura," aliwaambia waandishi habari katika mji mkuu, Harare.

Huku tarehe hii ikitangazwa, mwenyekiti wa tume inayosimamia uchaguzi, Simpson Mutambanengwe, alijiuzulu kwa sababu za kiafya.

Waziri mkuu Morgan Tsvangirai alisema kwamba kura hiyo itadhihirisha hatua muhimu kwa mageuzi ya kidemokrasia, shirika la habari la AFP limeripoti.

Kura hii itafuatiwa na uchaguzi mkuu utakaokuwa kati ya Bwana Tsvangirai na Rais Robert Mugabe.

Mugabe, 88, ameitawala Zimbabwe tangu ipate uhuru mwaka 1980.

Habari zaidi kuhusu katiba hiyo mpya, iliyokubaliwa na Bwana Mugabe na Bwana Tsvangirai, hazijatolewa rasmi, lakini kuna tetesi kwamba mihula ya urais itakuwa miwili tu.

Uchaguzi mkuu

Bwana Mugabe na Bwana Tsvangirai wanategemewa kuwasihi wapiga kura kukubali katiba hiyo. Hilo likitokea basi uchaguzi mkuu utafanywa chini ya katiba hiyo mpya.

Uchaguzi huo utaashiria hatima ya hali ya wasiwasi na utata iliyokithiri wakati viongozi hao wawili walipoamua kuunda serikali ya muungano baada ya uchaguzi wa 2008 uliozusha ubishi mkali wakati Bwana Tsvangirai aliposusuia duru ya pili ya uchaguzi alipodai kwamba ushindi wake ilikuwa umeibwa katika duru ya kwanza.

Tsvangirai ni kiongozi wa Movement for Democratic Change (MDC). Chama cha Bwana Mugabe cha Zanu-PF nacho kilinyooshewa kidole cha lawama kwamba kilizusha vurugu dhidi ya wafuasi wa MDC, dai ambalo ilikana.

Vyama hivyo viwili hatimaye viliamua kuunda serikali ya muungano, baada ya kushinikizwa kufanya hivyo na viongozi wa eneo la kusini mwa Africa.

Duru zinasema kwamba uchaguzi mkuu unapangwa kufanyika kati ya 15 na 30 Julai.