Al Shabaab wadai kumuua Mkenya

Image caption Al Shabaab wanataka serikali iwaachilie wafungwa wa kiisilamu wanaodaiwa kuwa magaidi

Wanamgambo wa Al Shabaab wanadai kumuua mateka Mkenya awaliyekuwa wanamzuilia baada ya Kenya kukosa kutimiza matakwa yao.

Al Shabaab wanaitaka serikali ya Kenya kuwaachilia huru waisilamu wanaozuiliwa nchini humo kwa tuhuma za ugaidi.

Wanamgambo hao, wanaotaka kutekeleza sheria za kiisilamu pia walisema kuwa wanaongeza makataa ya kuwaua mateka wengine wakenya kwa masaa 72 kuipa muda Kenya kutimiza matakwa yao.

Mapema mwezi Januari, wanamgamba hao walipatia Kenya makataa ya wiki tatu kuwaachilia wafungwa hao , lakini Kenya ikakataa kutimiza.

Kabla ya makataa hiyo kutolewa, wanamgambo hao walimuua mwanajeshi wa Ufaransa, waliyekuwa wanamzulia kama hatua ya kulipiza kisasi kile wanachosema ni mateso yanayofanyiwa na Ufaransa dhidi ya wapiganaji wa kiisilamu Mali.

Hata hivyo jeshi la Kenya linasema kuwa halinaufahamu wowote wa mwanajeshi wake kutekwa nyara na Al Shabaab.

Wadadisi wa maswala ya usalama, wanasema Al Shabaab ni kundi linaloishiwa na nguvu na kuwa halina udhibiti mkubwa wa sehemu kubwa ya Somalia. Pia sio tisho kubwa kwa wanajeshi wa Muungano wa Afrika wala wanajeshi wa Kenya.