Hatma ya washukiwa wa ICC kugombea Kenya

Image caption Uamuzi kuafikiwa ikiwa wawili hawa watawania nyadhiza za rais na makamu wake

Mahakama kuu nchini Kenya imeeleza kwamba haiwezi kuamua iwapo Uhuru Kenyatta na William Ruto wanapaswa kugombea nyadhifa katika uchaguzi mkuu ujao.

Wawili hao wanakabiliwa na tuhuma za kuchochea ghasia nchini Kenya baada ya uchaguzi uliokumbwa na utata na kusababisha mapigano ya kikabila.

Ikiwa zimesalia wiki mbili tu kwa uchaguzi mkuu kufanyika Kenya, inaonekana kuwa wananchi ndiyo watakaoamua kupitia kura, iwapo Uhuru Kenyatta na William Ruto wanafaa au hawafai kuwa viongozi nchini.

Uhuru Kenyatta anawania urais katika uchaguzi mkuu utakaokuja katika muda wa wiki mbili zijazo na makamu wake ni William Ruto.

Kesi hiyo iliwasilishwa na mashirika yasiyo ya serikali yaliyotaka kubainishiwa iwapo viongozi hao wawili wa muungano wa kisiasa, Jubilee, wana uwezo wa kuhudumu katika ofisi ya serikali wakati wanatuhumiwa kwa kesi za uhalifu.

Hali ambayo mashirika hayo yanaona ni kwenda kinyume na katiba ya nchi.

Mahakama ilikuwa iangalie iwapo Uhuru na Ruto wangechaguliwa, wataweza kutimiza jukumu la kuiongoza nchi, wakati wanatuhumiwa kwa kuhusika na ghasia zilizoshuhudiwa Kenya baada ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2007, katika mahakama ya uhalifu ICC, mjini Hague Uholanzi.

Uamuzi huu umetolewa baada ya hapo jana kuwepo kikao cha mahakama hiyo ya uhalifu ICC, kukagua hali ya kesi hiyo inayowakabili wawili hao.

Kesi hiyo iliyowasilishwa na mashirika yasiyo ya kiserikali inaendelea katika mahakama kuu mjini Nairobi na inatarajiwa kutoa uamuzi iwapo mahakama ina uwezo wa kutoa uamuzi juu ya wawili hao au iwapo itahitaji usaidizi wa mahakama ya juu nchini kufikia uamuzi kuhusu hilo.

Zimesalia wiki mbili tu kwa uchaguzi mkuu kufanyika Kenya na uamuzi huu huenda ukawa na athari kubwa kwa uchaguzi ujao.

Mahakama inajaribu kuona iwapo Uhuru na Ruto ikiwa watachaguliwa wataweza kutimiza jukumu la kuiongoza nchi, na wakati huo huo kukabiliana na kesi inayowaandama katika mahakama ya uhalifu wa kivita ICC mjini Hague Uholanzi, ambapo wanatuhumiwa kuhusika na ghasia zilizoshuhudiwa baada ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2007.