Usafishaji wafuatia kimondo Urusi

Maelfu ya wasaidizi, mafundi wa madirisha na watu waliojitolea wameshughulika na kazi kubwa ya kusafisha katika eneo la milima ya Ural nchini Urusi, baada ya kimondo kuripuka angani hapo jana na kuporomoka juu ya eneo hilo.

Watu zaidi ya 1,000 walijeruhiwa katika mripuko huo.

Wengi waliumizwa na gilasi kutoka madirisha yaliyopasuka kwenye shindo hilo karibu na mji wa Chelyabinsk.

Baridi Ijumaa usiku ilikuwa kali Chelyabinsk, nyuzi za baridi -20.

Kwa hivo wasaidizi na watengeneza madirisha wanapelekwa huko kwa ndege ili kuweka gilasi mpya kwenye madirisha yaliyovunjika majumbani mwa watu.

Hadi sasa jabali hilo liloporomoka kutoka angani halikupatikana kwa sababu liliangukia ndani ya ziwa liloganda barafu.

Wana-sayansi wanafikiri hilo ndilo jabali kubwa kabisa kuporomoka ardhini kwa zaidi ya karne moja.

Wanasayansi wa Marekani wa shirika la NASA wanafikiri uzito wake ni tani 7,000 huku wanasayansi wa Urusi wanadhani ni tani 10.