Ansaru wadai kuwateka nyara wafanyakazi Nigeria

Ramani ya Nigeria na jimbo la Bauchi

Kundi la wapiganaji la Ansaru, limedai liliwateka nyara wafanyakazi saba wa kigeni na kumuua mlinzi wakati wa tukio hilo .

Wafanyakazi kutoka Uitalia, Ufilipino, Uingereza, Ugiriki na Lebanon yasemekana ni kati ya wale waliotekwa nyara katika jimbo la Bauchi Kaskazini mwa Nigeria.

Wafanyakazi hao walikuwa kazini katika kiwanda kimoja wakati wapiganaji hao walipowateka nyara siku ya Jumapili.

Awali leo, polisi nchini walianzisha msako dhidi ya watu waliowateka nyara wafanyakazi hao.

Mlinzi katika kampuni hiyo ya ujenzi, Septraco, inayomilikiwa na watu wenye asili ya Lebanon, alipigwa risasi na kuuwawa kwenye ua la kampuni hiyo.

Septraco inapanua barabara moja kuu katika jimbo la Bauchi. Awali, kituo cha polisi katika mji wa Jama'are kilishambuliwa na magari mawili kulipuliwa.

Mapema mwezi huu, watoa chanjo za polio tisa walipigwa risasi na kuuwawa katika zahanati mbili hukuhuko kaskazini mwa Nigeria.

Kudni la Ansaru ambalo lieanza harakati zake mwezi Juni mwaka jana, iliwatumia wandishi wa habari barua pepe kusema kuwa hao ndio waliohusika na kitendo hicho.

Wizara ya mambo ya nje ya Uingereza hata hivyo ilikimya kuhusu ikiwa raia wa Uingereza alikuwa miongoni mwa wale waliotekwa nyara.

Visa vua utekaji nyara ni jambo la kawaida nchini Nigeria hasa watu matajiri na wafanyakazi wa kigeni ndio hulengwa sana.