Waangalizi wa EAC Kenya

Jumuiya ya Afrika Mashariki hii leo imezindua rasmi kikundi chake cha waangalizi wa uchaguzi wa Kenya zikiwa zimesalia wiki mbili kabla ya uchaguzi wenyewe kufanyika.

Kikundi hicho kitakuwa na waangalizi 40 katika uchaguzi huo utakaofanyika tarehe 4 Machi.

Waangalizi hao wataongozwa na Abdurrahman Kinana, kiongozi anayesifika Afrika Mashariki na spika wa zamani wa bunge la Afrika Mashariki.

Kwa mujibu wa Jumuiya hiyo, kuletwa Kenya kwa waangalizi wa Jumuiya ya Afrika mashariki ni sehemu ya kazi ya jumuiya hiyo kudumisha Demokrasia na uongozi bora sambamba na misingi bora kwa jumuiya ya Afrika Mashariki.

Wajumbe hao wanatoka katika nchi zote za Afrika Mashariki na wanahusika na maswala mbali mbali kuhusu uandaaji wa uchaguzi pamoja na utakavyoendeshwa.

Ni pamoja na wajumbe kutoka bunge la Afrika Mashariki, tume za uchaguzi, tume za kitaifa za haki za binadamu na waakilishi wa maswala ya vijana. Uteuzi wa waangalizi hawa, ulizingatia usawa wa kijinsia pamoja na kuwahusisha vijana.

Jukumu halisi la waangalizi hawa ni kuhakikisha Kenya inaandaa uchaguzi huru na wa haki, kwa hali iliyo salama na thabiti.

Wakenya watakuwa wanamchagua rais mpya, waakilishi katika bunge la senate na bunge la waakilishi pamoja na magavana wa kaunti arobaini na saba, waakilishi wa wanawake na makansela.

Tayari, muungano wa ulaya una waangalizi wake nchini humo. Kenya ni muhimu kwa Jumiya ya Afrika Mashariki kwani ndiyo nchi yenye uchumi mkubwa katika kanda hiyo,

Wafanyabiashara wengi wa Kenya huendesha biashara zao katika karibu nchi zote jirani.

Na kwa hivyo, kwa sababu ni sehemu ambapo nchi za afrika Mashariki zinaitumia kama kiingilio cha bidhaa zao, usalama na uthabiti wa nchi hiyo ni muhimu kwa kanda yote hasa wakati huu wa uchaguzi.