Rais Correa ashinda uchaguzi Ecuador

Rais Correa
Image caption Rais Correa

Rais wa Ecuador Rafael Correa amechaguliwa tena kwa mara ya tatu. Alipata zaidi ya asilimia 50 ya kura zilizopigwa. Mpinzani wake mkuu alikubali kushindwa.

Matokeo ya muda yalionyesha kuwa Bwana Correa alipata asilimia 56.6, huku mpinzani aliyemkaribia, Guillermo Lasso, akipata asilimia 24. Wagombeaji wengine hawakutegemewa kupata zaidi ya asilimia 5.

Akiwahutubia wafuasi wake katika mji mkuu, Quito, Bwana Correa aliashiria kwamba kungekuwa na "miaka mingine minne ya mageuzi ".

Alichaguliwa kwa mara ya kwanza mnamo 2007. Kiongozi huyu wa kisosholisti alileta utulivu wa kisiasa katika nchi nchi iliyokuwa imekumbwa na miongo kadhaa ya vurugu na mapinduzi ya serikali.

Lakini wapinzani wake wanasema kwamba Bwana Correa ana ishara za kuwa dikteta.

Correa, ambaye ni mtaalam wa uchumi, amelaumiwa kwa kuanzisha sera ambazo zimejenga utalwala wake na kupunguza zile za wapinzani wake wa siasa, na vyombo binafsi vya habari.

Lakini maguezi yake, yaliyojulikana kama "maguezi ya wananchi", yamempa umaarufu na wananchi wa kawaida wa Ecuador, na kumwezesha kujenga urafiki na viongozi wengine wa mrengo wa kushoto wa Amerika Kusini.