Hafla kuhusu turathi za Mali yafanywa

Image caption Waasi wapiganajji wakivunja kaburi la zamani mnamo 1 Julai 2012

Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni, UNESCO, leo linaandaa siku ya tamasha na mikutano ili kujadili suala la uhifadhi wa makavazi ya kihistoria ya Mali.

UNESCO sasa inapanga kuwatuma wataalamu wa kihistoria ili kuchunguza ni nini kinachohitajika ili kuhifadhi sehemu zilizobaki.

UNESCO inasema kuwa makaburi 11 maarufu mjini Timbuktu yaliteketezwa na waasi wa Kiisilamu, huku vitabu vya kumbukumbu pia vikiharibiwa. Kwa bahati nzuri hata hivyo, yapo makaburi muhimu yaliyonusurika.

Waziri wa utamaduni nchini Mali, Bruno Maiga, ataungana na ujumbe kutoka umoja huo katika hafla hii. Lengo lake ni kuwahamasisha watu kuhusu uharibifu uliofanyiwa turathi za Mali mijini Timbuktu na Gao wakati wa mapigano ya takriban mwaka mmoja.

Waasi wa Kiisilamu waliyachoma makaburi hayo kwa madai kwamba yanatumiwa kwa matambiko ya kishirikina, kinyume na mafunzo ya dini ya Kiislamu.