Watalii 7 wametekwa nyara Cameroon

Watu waliokuwa wamejihami nchini Cameroon wamewateka nyara watalii saba karibu na mpaka wa Nigeria . Ni kwa mujibu wa rais wa Ufaransa , Francois Hollande.

Anasema kuwa ni watu wa familia moja na walitekwa nyara na kundi la kigaidi ambalo lina mizizi yake Nigeria.

Rais Hollande aliongeza kuwa watalii hao huenda walipelekwa Kaskazini mwa Nigeria.

Makundi mawili ya wapiganaji wa kiisilamu, huendesha sana harakati zao katika eneo hilo.

Kundi moja la Ansaru, lilidai kuwateka nyara wafanyakazi saba wa kigeni waliokuwa wanafanya kazi katika kiwanda kimoja eneo hilo siku ya Jumapili.

Wafanyakazi hao walikuwa ni pamoja na raia wa Italia, Uingereza, na Lebanon, wanaoaminika bado kuwa mikononi mwa wapiganaji wa Ansaru katika jimbo la Bauchi.

Ansaru pia wanasema wamemteka raia wa Ufaransa Francis Colump, aliyekamatwa katika jimbo la Katsina.

Kundi lengine la wapiganaji wa kiisilamu,Boko Haram, limekuwa likiwateka nyara watu katika maeneo ya Kaskazini mwa Nigeria katika miaka ya nyuma.

Afisaa mmoja wa usalama nchini Cameroon alisema kuwa watalii hao walikuwa wanarejea nyumbani kutoka mbuga ya wanyama ya Waza walipovamiwa.