Jumuiya ya Madola yazungumzia uchaguzi Kenya

Image caption Bendera za nchi ya Jumuiya ya madola

Baraza la Jumuiya ya Madola Alhamisi lilisema kwamba linategemea kwamba uchaguzi nchini Kenya mwezi ujao utafanywa vizuri kama ilivyofanywa kura ya maoni ya mwaka 2010 kwa njia ya haki.

Katibu Mkuu wa Jumuiya hiyo Kamalesh Sharma alisema kwamba uchaguzi huo utaipa Kenya fursa ya kuhakikisha kuwa vurugu kama zilizoshuhudiwa 2008 hazitokei tena.

Jumuiya hiyo ilitangaza kuwa imeshatuma waanglizi 17, wanaoongozwa na rais wa zamani wa Botswana Festus Mogae.

Bwana Sharma alisema : “Tunategema kwamba pande zote zitadumisha amani.”

Mbali na kikundi hicho, tayari wameshawasili waangalizi wengine wa kimataifa kama wale wa Muungano wa Nchi za Ulaya, ambao wameshasambazwa kote nchini.

Mwenyekiti wa tume ya uchaguzi, IEBC, Ahmed Issack Hassan amesema kwamba wameshazialika tume kutoka Ghana, Nigeria na Afrika Kusini zije kushuhudia uchaguzi huu.

Balozi za Marekani na Uingereza nazo pia zimeshatuma waangalizi wao.