Wafanyakazi wa Umma wagoma Malawi

Image caption Mojawapo ya mashirika yaliyoathirika ni shirika la ndege la Kenya

Viwanja vya ndege nchini Malawi, vimefungwa kufuatia mgomo wa wafanyakazi wa umma wakidai nyongeza ya mishahara.

Safari za ndege za kimataifa na za kikanda, zilisitishwa kulingana na mwandishi wa BBC mjini Blantyre Raphael Tenthani .

Mgomo huo, unaosemekana kuathiri pakubwa karibu idara zote za serikali, ndio mkubwa zaidi kuwahi kufanyika tangu kuingia mamlakani kwa rais Joyce Banda mwaka jana .

Bi Banda, ambaye bado hajazungumzia mgomo huo, anatarajiwa kusafiri Equatorial Guinea baadaye leo.

Hata hivyo haijulikani ikiwa ataendelea na ziara yake huku viwanja viwili vya kimataifa vya ndege mjini Blantyre na Lilongwe, vimefungwa.

Wanaosafiri kwa ndege za mashirika ya ndege ya Afrika Kusini, Kenya na Ethiopia walitatizika Jumatano

Takriban wafanyakazi 120,000 wa umma, ikiwemo walimu na wafanyakazi wa umma, wanagoma , wakidai kuongezwa mishahara ili kumudu gharama inayopanda ya maisha .

Wafanyakazi walilalamika kuwa tangu serikali kushusha hadhi ya sarafu ya nchio hiyo, Kwacha, kwa asilimia 49 mwezi Mei, mishahara yao imeathiriwa vibaya.

Mnamo Alhamisi, waziri wa fedha Ken Lipenga, alisema kuwa serikali haina uwezo wa kuongeza mishahara ya umma

'Mabango ya kumpinga Banda'

Mashirika ya wafanyakazi wa umma, yanataka asilimia 65 ya nyongeza ya mishahara karibu mara mbili ya mfumuko wa bei nchini humo.

Image caption Joyce Banda anatarajiwa kugombea urais kwa mara ya kwanza tangu kifo cha mtangulizi wake Bingu wa Mtharika

Mgomo ulianza wiki jana, lakini sasa umekithiri huku shule za umma pia zikiathiriwa.

Wafanyakazi pia walifanya maandamano wakiipinga serikali wakiwambia rais Banda kamwe hawatampigia kura.

Utakuwa uchaguzi wa kwanza kwa Joyce Banda kugombea tangu aingie mamlakani, kufuatia kifo cha mtangulizi wake Bingu wa Mutharika, mwezi Aprili, mwaka jana.

Uliokuwa utawala wa Mutharika, ulikumbwa na maandamano ya kupinga gharama ya maisha na kupanda kwa bei ya mafuta.

Wajumbe wa shirika la fedha duniani, IMF,walimaliza ziara yao nchini Malawi.

Afisaa mkuu wa shirika hilo nchini Malawi, alisema kuna dalili nzuri kuwa uchumi wan chi hiyo unaimarika.