Kesi ya dhamana ya Pistorius kuamuliwa

Image caption Pistorius anasema hakumuua mchumba wake kwa maksudi

Jaji nchini Afrika Kusini hii leo anatarajiwa kutoa uamuzi ikiwa mwanariadha mlemavu Oscar Pistorius, anayetuhumiwa kwa mauaji ya mchumba wake, anaweza kuachiliwa kwa dhamana.

Mwanariadha huyo anakanusha kosa la mauaji akisema kuwa alimpiga risasi Reeva Steenkamp akidhania kuwa alikuwa jambazi.

Upande wa utetezi unasema kuwa ushahidi huo wenye utata na uliotolewa na mmoja wa polisi umeweza kuhujumu upande wa mashtaka.

Hata hivyo upande wa mashtaka unasema kuwa kuna hofu kuwa Pistorius huenda akakosa kufika mahakamani ikiwa ataachiliwa kwa dhamana.

Pistorius anatarajiwa kurejea katika mazoezi wiki ijayo,ikiwa atapewa dhamana.

Kocha wake aliyasema hayo alipowasili mahakamani kwa siku ya nne ya kusikiliza kesi ya dhamana dhidi ya Pistorius.

Mnamo Alhamisi polisi walimbadilisha jasusi aliyekuwa anachunguza kesi hiyo na kuweka polisi mwingine baada ya taarifa kujitokeza kuwa polisi huyo mwenyewe alikuwa anakabiliwa na kesi ya jaribio la mauaji.

Jasusi mkuu wa Afrika Kusini Luteni, Vineshkumar Moonoo, ndiye atachunguza kesi hiyo sasa.

Viongozi wa mashtaka wanasema kuwa Pistorius alifyatua risasi nne katika bafu yake iliyokuwa imefungwa huku marehemu Steenkamp akiwa ndani. Aligongwa kichwani , kwenye paja na mkononi.