Wamisri waambiwa wasusie uchaguzi

Kiongozi wa upinzani nchini Misri, Mohammed ElBaradei, ametoa wito kuwa watu wasusie uchaguzi ujao wa wabunge unaotarajiwa kufanywa mwezi ujao.

Katika ujumbe kwenye mtandao wa Twitter, Bwana ElBaradei - anayeongoza chama cha National Salvation Front - alisema anakariri wito ule-ule aliotoa wakati wa uchaguzi wa mwaka wa 2010, kama njia ya kuonesha kuwa demokrasi ya Misri ni ya uongo.

Rais Morsi alitangaza uchaguzi huo awali juma hili, na yeye na chama chake cha Muslim Brotherhood wanatumai hatua hiyo itasaidia kumaliza maandamano ya miezi kadha.

Lakini upinzani unasema hilo ni jaribio jipya la kuhakikisha chama cha Kiislamu kinashikilia madaraka.