Watu zaidi ya 50 wauwawa Darfur

Wanajeshi wa Umoja wa Mataifa Darfur

Umoja wa Mataifa nchini Sudan unasema mauaji ya watu zaidi ya 50 yaliyotokea Jumamosi kaskazini mwa Darfur ni pigo jengine dhidi ya juhudi zake za kusambaza msaada kwa maelfu ya watu waliokimbia ghasia za kikabila za hivi karibuni.

Damian Rance wa ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Ushirikiano na Msaada alisema misafara ya misaada ilizuwiliwa kuingia mji wa El Sireaf, ambao ulishambuliwa na kundi la wanamgambo wa Kiarabu.

Inakisiwa kuwa watu kama laki moja wamekimbia makwao katika jimbo la Darfur Kaskazini tangu awali mwezi wa Januari wakati ghasia zilipozuka kuhusu haki ya kuchimba madini baina ya makundi ya Waarabu yanayozozana.

Juma hili inatimia miaka 10 tangu vita vya Darfur kuanza.

Watu karibu milioni moja na nusu wa Darfur wanaishi kwenye makambi ya wakimbizi.