ICC huenda ikaakhirisha kesi ya Kenya

Image caption Uhuru na Ruto wakiendesha kampeini zao za uchaguzi

Viongozi wa mashtaka katika mahakama ya kimataifa ya ICC, wamesema kuwa hawapingi kuakhirishwa kwa kesi ya wakenya mashuhuri walioshtakiwa kwa kuchochea ghasia za baada ya uchaguzi mkuu wa 2007.

Mmoja wa washukiwa hao ni Uhuru Kenyatta ambaye ni naibu waziri mkuu na anagombea urais katika uchaguzi mkuu utakaofanyika Jumatatu.

Kesi inayomkabili Kenyatta na mgombea mwenza wake William Ruto, ilitarajiwa kufanyika mwezi Aprili.

Lakini upande wa utetezi ulilalamika kuwa hawakupewa muda wa kutosha kujiandaa kwa kesi hiyo.

Msemaji wa ICC Fadi El Abdallah, alisema kuwa majaji bado hawajaamua ikiwa wataikhirisha kesi hiyo au la.

Lakini viongozi wa mashtaka wanasema kuwa huenda kesi hiyo ikaakhirishwa hadi mwaka ujao.

Awali viongoizi wa mashtaka walikataa kuikhirisha kesi hiyo lakini wanaitikia kuwa huenda ikawa vigumu kuiendesha kwa sababu ya tatizo la kupatikana kwa nafasi kwenye mahakama hiyo ya kuendeshea kesi.

Athari za kisiasa za kucheleweshwa kwa kesi hiyo zitakuwa muhimu ikiwa hapatakuwa na mshindi bayana na kulazimika kufanyika kwa duru ya pili.

Pia itamaanisha kuwa washtakiwa watakuwa huru kusalia Kenya na kushiriki katika duru ya pili.

Bwana Kenyatta na mgombea mwenza wake William Ruto, wanashtakiwa kwa kufanya uhalifu wa kivita kufuatia ghasia za baada ya uchaguzi 2007, ambao uliwaacha zaidi ya watu elfu sita kuuawa na wengine elfu moja na zaidi kuachwa bila makao.

Balozi wa zamani wa kenya katika Umoja wa Mataifa, Francis Muthaura na mwandishi wa habari, Joshua arap Sang wanakabiliwa na makosa sawa na hayo ICC.