Gbagbo''nilikuwa mpigania demokrasia''

Image caption Wafuasi wa Gbagbo walikuwa mahakamani kusikiliza kesi dhidi yake

Rais wa zamani wa Ivory Coast Lurent Gbagbo, ameambia mahakama ya kimataifa ya uhalifu wa kivita ICC kuwa daima amekuwa akipigania demokrasia.

Mahakama hiyo itaamua ikiwa Gbagbo ashtakiwe kwa kosa la uhalifu wa kivita kufuatia ghasia za baada ya uchaguzi nchini humo miaka miwili iliyopita.

Takriban watu 3,000 waliuawa katika ghasia hizo baada ya Gbagbo kukataa ushindi wa mpinzani wake.

Gbagbo mwenye umri wa miaka 67, yuko katika mahakama ya ICC na anasisitiza kuwa hana hatia.

Haya ndiyo yalikuwa matamshi yake ya kwanza mahakamani tangu mwezi Disemba mwaka 2011 alipofikishwa huko.

Mwandishi wa BBC mjini Hague, Anna Holligan, amesema kuwa Gbagbo aliongea kwa dakika kumi na tano, kama mwanasiasa mkakamavu kuliko mtu anayekabiliwa na makosa katika mahakama ya ICC.

Wafuasi wake walikuwemo ndani ya mahakama.

Gbagbo aliambia mahakama kuwa yeye siyo tajiri mkubwa wala kuwa na kipawa kuwashinda wengi na kwamba aliingia katika siasa kujitolea kupigania demokrasia.

Alikuwa rais wa Ivory Coast kutoka mwaka 2000 hadi alipokamatwa mwezi Aprili mwaka 2011, baada ya kukataa kukubali kuwa alishindwa na mpinzani wake Alassane Ouattara.

Aidha serikali ya rais Ouattara ilimkabidhi Gbabgbo kwa mahakama ya ICC na inaituhumu Ufaransa,nchi iliyokuwa mkoloni wa Ivory Coast kwa njama ya kutaka kumng'oa mamlakani.

Mahakama ya ICC, ilianza kufanya kazi mwaka 2002 kujaribu kuwachukulia hatua washukiwa wa uhalifu wa kibinadamu pamoja na uhalifu wa kivita kote duniani.

Gbagbo ni rais wa zamani wa kwanza kuzuiliwa katika mahakama ya ICC, ingawa Slobodan Milosevic wa Yugoslavia na rais wa zamani wa Liberia Charles Taylor walifikishwa katika mahakama maalum ya ICC.