Kenya yafanya kampeni za mwisho

Wagombea uchaguzi wa Kenya wanafanya mikutano ya mwisho ya hadhara kabla ya upigaji kura Jumatatu.

Huu ndio uchaguzi wa kwanza kufanywa kufuatana na katiba mpya ambayo inalenga kuepusha ghasia zilizotokea miaka mitano iliyopita.

Mjini Nairobi maelfu wamekusanyika katika uwanja wa Nyayo kumsikiliza Waziri Mkuu, Raila Odinga.

Wafuasi wa Naibu Waziri Mkuu Uhuru Kenyatta wako katika uwanja wa Uhuru.

Huku nyuma Wakenya walioko nchi za n'gambo wanasema wanaona wameonewa kwa kutoruhusiwa kupiga kura, ingawa fedha wanazopeleka nyumbani zinasaidia sana uchumi wa nchi yao.

Inakisiwa kuwa Wakenya walioko nje, hasa Marekani, Uingereza, Ujerumani na nchi jirani ni kama milioni mbili na nusu.

Mwezi Novemba serikali ya Kenya iliamua kuwa Wakenya walioko nje ya nchi hawataweza kupiga kura kwa sababu ya matatizo ya usafiri na kifedha.