Uchaguzi wa Kenya:Matarajio yako

Image caption Maandamano ya kutaka wakenya kupiga kura kwa amani

Wakenya wanapiga kura Jumatatu , 4 katika uchaguzi wa kwanza tangu ghasia za baada ya uchaguzi mwaka 2007, ambazo zilisababisha vurugu za kikabila.

BBC imewahoji wakenya kutoka sehemu mbali mbali za nchi kuhusu matarajio yao na kile ambacho wanakiona kama changamoto zitakazomkabili rais mpya na serikali yake

Caroline Osik, Homabay

Swala nyeti katika uchaguzi wa Kenya wakati huu ni ujumbe wa amani. Serikali tayari imewahakikishia wananchi kuwa imeweka mikakati thabiti ya usalama katika maeneo yaliyokumbwa zaidi na ghasia za baada ya uchaguzi mwaka 2007. Sote tunatumai kuwa kutakuwa na usalama

Niliathirika wakati wa ghasia za baada ya uchaguzi kwani naishi katika eneo ambalo lina mgawanyiko mkubwa kuhusu ukabila. Lakini hatukutarajia kuwepo ghasia wakati huo.

Watu wengi wameamua nani watampigia kura, nafikiri mijadala miwili ya wagombea wa urais ilisaidia wananchi kuamua watakayempigia kura.

Kwenda katika mfumo mpya wa Kaunti, ni kitu kipya kwetu na itakuwa changamoto kwa mara ya kwanza. Tutakuwa na magavana , maseneta watakaochukua nyadhifa kwa mara ya kwanza. Sasa tunastahili kujiandaa kwa mfumo mpya wa uongozi

Joshua, Nairobi

Joshua Kwendo

Mwaka 2007 uliathiri sana nchi yetu. Kulikuwa na tatizo la kupata mahitaji muhimu kote nchini.

Maswala makuu katika uchaguzi huu ni ardhi na ufisadi. Licha ya kuwa na sheria kali dhidi ya ufisadi, lakini bado ni changamoto kubwa katika baadhi ya taasisi za serikali na taasisi za umma kama idara ya polisi.

Pia tulipitisha katiba ambayo ina mageuzi makubwa na wakenya wanataka sana iweze kutekelezwa.Na kwa sababu ya kuwepo tume huru ya uchaguzi na mipaka pamoja na hii katiba mpya, inawezekana ni vigumu kutokea tena ghasia.

Anna, Mombasa

Anna,Mombasa

Watu wengi nchini Kenya, wanataka uchaguzi wa amani.

Ghasia za baada ya uchaguzi mkuu mwaka 2007, hazikuwa jambo jipya, pia zilishuhudiwa miaka ya tisini.Ni jambo ambalo hutokea kila baada ya miaka mitano.

Labda ni kwa sababu tuu ghasia za mwaka 2007 zilikuwa kwa kiwango kikubwa ndio maana zikapigwa daruibini sana.

Sidhani kama kuta kuwa na wizi wa kura wakati huu, kwa sababu kutakuwa na waangalizi wa kimataifa.

Mjini Mombasa kuna mchanganyiko wa makabila na watu kutoka Kenya yote waliozaliwa mjini humo. Watu hapa wanahisi kama wametengwa na ndio maana huwa hawajisajili kupiga kura.

Corrie Kisilu,Nairobi

Najiandaa kupiga kura. Naamini uchaguzi huu utakuwa uamuzi mkubwa kwa sababu uchaguzi wa 2007 ulikumbwa na ghasia.

Hakuna mkenya anayetaka kushuhudia yaliyokea mwaka huo.

Swala linalomkabili Uhuru Kenyatta na mgombe wake, William Ruto, ni swala tete hasa kwa wale wanaoelewa athari za kuwachagua wawili hao.

Lakini tatizo ni kwamba watu wengi hawajaelimishwa kuhusu athari za kuwa na rais anayetakiwa na mahakama ya ICC

Ikiwa mgombea ninayemtaka hatashinda, nitakubali tu kushindwa kwa sababu mabadiliko yanaanza na mimi kama mpiga kura.

Joseph, Kitale

Nitapiga kura Jumatatu kumchagua kiongozi ninayemtaka na ambaye nahisi ataongoza nchi hii kuweza kufikia ndoto yake, kiongozi atakayelinda katiba mpya, kiongozi au viongozi watakaohakikisha tunafanikiwa kutekeleza maono yetu.

Maoni yangu kuhusu uchaguzi wa mwaka huu, ni kwamba utakuwa na ushindani mkubwa na kwamba wakenya wataushiriki kwa amani.

Nina uhakika ghasia hazitatokea tena kwa sababu idara ya mahakama imefanyiwa mageuzi makubwa na hata idara ya polisi ingali inafanyiwa mageuzi na angalau inawezea kusemekana kuwa huru kwa sasa. .

Tatizo la uchaguzi mkuu wa 2007, halikuwa wapiga kura , ilikuwa viongozi ambao walihusika kwa njia moja au nyingine kuchochea ghasia.

Lakini wakenya wamezinduka baada ya kilichotokea. Hakuna mtu yuko tayari kuanza kumuua mwenzake.

Nina matumaini makubwa sisi ndio tutakuwa washindi kama wakenya kwani mshindi kati ya wagombea anaweza kuwa tu mmoja na ni matumaini yangu kuwa mshindi ataunganisha wakenya.