Wakenya wapiga kura ya kihistoria

Image caption Wapiga kura walisubiri kwa muda mrefu kabla ya kupiga kura

Wakenya wangali wanapiga kura licha ya muda wa mwisho wa shughuli hiyo kutimia.Upigaji kura ulianza asubuhi na mapema baadhi ya wagombea wakiwa katika vituo vya kupiga kura saa nane na saa tisa usiku.

Mwandishi wa BBC Ann Mawathe anasema kuwa katika kituo kimoja mjini Kisumu, bado mamia ya wapiga kura wamepiga foleni wakisubiri kupiga kura.

Kulingana na tume ya uchaguzi mkuu, kila mpiga kura ambaye angali kwenye foleni hata baaya ya muda kukamilika, ataruhusiwa kupiga kura, lakini hakuna watu wataruhusiwa kujiunga na foleni kupiga kura.

Baadhi ya vituo vya kupigia kura vimefunga rasmi shughuli ya kupiga kura baada ya muda wa mwisho wa shughuli hiyo kutimia.

Milolongo mirefu ilishuhudiwa katika sehemu nyingi za nchi baadhi zikiwa hata karibu kilomita moja, ishara ya walivyojitokeza wakenya kwa shughuli hiyo ambayo ni ya kihistoria.

Kuna hofu kuwa huenda shughuli hiyo ikaendelea hadi usiku kwani milolongo bado ni mirefu sana.

Kwa hili kuna taarifa kuwa baadhi ya wagombea wanapinga swala la kuendelea na shughuli ya kupiga kura kwa hofu ya wizi wa kura.

Image caption Karani wa uchaguzi katika moja ya vituo vya kupigia kura mjini Nairobi

Usalama ulidhibitiwa kote nchini polisi wakiwekwa katika sehemu mbali mbali, kuhakikisha wapiga kura wanaendelea na shughuli katika mazingira salama.

Katika sehemu mbali mbali kulikuwa na visa vya vurugu mfano mjini Mombasa ambako wanachama wa kundi la MRC waliwashambulia polisi waliokuwa wanashika doria na kuwaua wanne.Pia waliwaua raia kadhaa wasiokuwa na hatia.

Lengo la kundi hilo lilikuwa kuvuruga uchaguzi mjini Mombasa pwani ya Kenya.

Kundi hilo limekuwa likitaka uhuru wa jimbo hilo kwa madai kuwa wametengwa na serikali.

Magombea wa urais Raila Odinga aliwataka wananchi kustahimiliana pamoja na kuwapongeza kwa kupiga kura kwa utulivu.

Image caption Akina mama waliokuwa na watoto waliruhusiwa kupiga kura bila kupanga foleni

Naye Uhuru Kenyatta alisikitika na matukio ya Mombasa na kuwambia wakenya kuwa watulivu pia.

Mwandishi wa BBC Emmanuel Igunza anasema kuwa foleni mjini Nakuru zimeanza kupungua na huenda wapiga kura wakamaliza shughuli hiyo itimiapo saa kumi na moja jioni muda wa mwisho wa kupiga kura

Matokeo ya uchaguzi yanatarajiwa kutangazwa leo usiku ingawa tume ya uchaguzi ina hadi siku saba kutoa matangazo ya matokeo ya kura za urais.