Shule za mafunzo ya Qur'an kufungwa Senegal

Image caption Sehemu ya shule ya mafunzo ya dini iliyofungwa

Rais wa senegal Macky Sall, anasema kuwa serikali itafunga shule zote za mafunzo ya dini ambazo zitakosa kutimiza mahitaji ya usalama kwa watoto.

Matamshi yake Rais Macky Sall, yanajiri baada ya watoto tisa kufariki katika ajali ya moto katika shule iliyo karibu na mji mkuu wa nchi hiyo Dakar.

Moto huo, ulizuka wakati watoto 45 wa shule wenye kati ya umri wa miaka sita na kumi na mbili, wakiwa ndani ya chumba kimoja katika eneo la Medina.

Inaarifiwa huenda mshumaa ndio ulisababisha ajali hiyo ya moto uliozuka Jumapili jioni.

Baada ya kuzuru eneo la ajali, bwana Sall, alisema kuwa shule za mafunzo ya kidini ambazo zinawadhulumu watoto na kukosa kuhakikisha usalama wao, lazima zifungwe.

''Watoto watarejeshwa kwa familia zao,'' aliongeza rais Sall

Mwandishi wa BBC Thomas Fessy mjini Dakar, alisema kuwa makundi ya kutetea haki za binadamu, yalionya dhidi ya mazingira mabovu ambamo watoto wanaishi kama makaazi yao kwenye shule za mafunzo ya dini na baadhi ya walimu wanawadhulumu watoto.

Wanafunzi wengi wanajulikana kama "talibes" kwa lugha ya kiasili, na husihia kuomba omba chakula na pesa mitaani na kisha kuwapelekea walimu hao.