Wakimbizi wa Syria wafika milioni moja

Image caption Idadi ya wakimbizi inaendelea kuongezeka huku majirani wa Syria wakikabiliwa na wakati mgumu

Idadi ya wakimbi wanaotoroka vita nchini Syria imefika milioni moja , kulingana na umoja wa mataifa.

Kamishna mkuu wa shirika la kuwahudmia wakimbizi la UN , ameelezea kuwa idadi ya watu wanaotaka makao salama katika nchi jirani za Syuria imeongezeka tangu mwanzoni mwa mwaka huu.

Nusu ya wakimbizi ni watoto , wengi wakiwa chini ya umri wa miaka 11 na mara kwa mara wanaathirika sana kimawazo kutokana na hali ya mazingira wanamoishi.

Idadi kubwa zaidi ya wakimbizi wanatafuta makaazi nchini Jordan, Lebanon, Uturuki ,Iraq na Misri

"Syria inaelekea katika hali ya janga kubwa,'' alisema kamishna huyo wa wawakimbizi Antonio Guterres katika taarifa iliyotolewa kuonya kuwa uwezo wa jamii ya kimataifa kushughulikia janga hili umekuwa mdogo sana.

''Janga hili lazima likomeshwe,'' aliongeza bwana Guteres akionya kuwa idadi kubwa ya wakimbizi hao pia imetatiza uwezo wa nchi jirani kusaidia.

Wengi wa waliotoroka vita sasa wanaishi katika hali ngumu katika mazingira chafu na wanakabiliwa na uhaba wa taasisi za usaidizi.

Umoja wa mataifa unasema uhamiaji huo mkubwa umeongezeka katika wiki za hivi karibuni huku thuluthi moja ya idadi hiyo wakiwa wameyakimbia mapigano hayo tangu mwanzoni mwa mwaka huu.

Nchi jirani zinazowapokea maelfu ya wakimbizi hao kila siku , zinang'ang'an kukabiliana na hilo.

Na mashirika ya msaada yanalalamika kwamba yamepokea dola nusu bilioni tu kutoka kwa wafadhili wa kimataifa kuwasaidia wakimbizi hao wa Syria.