Mahakama Kenya yatupilia mbali kesi

Image caption Shughuli ya kuhesabu kura ambayo imechukua muda mrefu kuliko ilivyotarajiwa

Mahakama kuu nchini Kenya imetupilia mbali kesi iliyokuwa imewasilishwa na mashirika ya kijamii dhidi ya tume ya uchaguzi wakiitaka isitishe shughuli ya kuhesabu kura za urais.

Mahakama hiyo ilisema haina uwezo wa kuamua kesi hiyo na sharti ipelekwe katika mahakama ya juu zaidi kwa uamuzi.

Mashirika hayo chini ya mwavuli wa shirika la, Africa Centre for Open Governance (africog), yanataka shughuli hiyo kusitishwa wakidai kuwa tume ya uchaguzi inayahujumu matokeo.

Jopo la majaji waliotoa uamuzi huo, Isaac Lenaola, David Majanja na Weldon Korir, mapema leo walikuwa na kikao kujua mwanzo ikiwa mahakama ina uwezo wa kusikiliza kesi hiyo au la kabla ya kuweza kutoa uamuzi.