Mandela arudishwa hospitalini Pretoria

Image caption Mandela apelekwa hospitalini tena

Rais Mstaafu wa Afrika Kusini Nelson Mandela amepelekwa hospitalini kufanyiwa uchunguzi wa kiafya.

Taarifa kutoka kwa afisa ya Rais wa Afrika Kusini zimesema kuwa uchunguzi huo ni wa kawaida tu.

Kwa muujibu wa tovuti ya Urais, Madaktari wanaomfanyia uchunguzi Mzee Mandela wamesema hakuna haja ya kuwa na taharuki yeyote.

Kwa muda mrefu sasa hali ya kiafya ya rais huyo mstaafu imekuwa ni swala la kutia wasiwasi.

Mandela mwenye umri wa miaka 94 alilazwa hospitalini kwa siku 18 mwezi wa Desemba mwaka jana kutokana na kutatizwa na mapafu pamoja na vijiwe ndani ya kibofu chake cha mikojo.

Taarifa iliyoandikwa kwenye mtandao wa Ofisi ya Rais Jacob Zuma zimeeleza kuwa Mzee Mandela alipelekwa katika Hospitali ya Mjini Pretoria kwa uchunguzi wa kawaida wa ki-afya.

Taarifa hiyo imeendelea kusema kuwa hatua hiyo imechukuliwa kutokana na matatizo yanayoambatana na umri wake mpevu.

Mzee Mandela alihudumu kama rais wa Afrika Kusini kati ya mwaka 1994 hadi 1999 na ndiye rais wa kwanza mweusi kuwahi kuitawala nchi hiyo.

Kutokana na juhudi zake za kupigania demokraisa na kupambana na sera za ubaguzi wa rangi nchini humo, Mzee Mandela anatambulika kama Baba wa Taifa nchini Afrika Kusini.

Tangu mwaka 2004 Mzee Nelson Mandela amekuwa hajitokeza hadharani au kushiriki katika shughuli zozote za umma.