Binamu wa Gaddafi amekamatwa Misri

Image caption Muammar Gaddafi na Ahmed Al Dam

Polisi nchini Misri wamemkamata aliyekuwa mwandani wa Hayati kiongozi wa Libya Kanali Muammar Gaddafi.

Bwana Ahmed Gaddaf al-Dam ambaye pia ni binamu wa Gaddafi alikamatwa kufuatia msako mkali uliofanywa usiku kucha na polisi wa Misri.

Kabla ya harakati za kumpindua Kanali Gaddafi , Bwana Al-Dam kwa miaka mingi alikuwa ni balozi maalum wa Tripoli mjini Cairo lakini alitoroka mwaka wa 2011.

Ingawa jamaa huyo wa aliyekuwa kiongozi wa Libya anatakikana na utawala wa sasa nchini kwao lakini hadi sasa haijafahamika atashitakiwa kwa makosa gani.

Kabla ya kukamatwa kwake katika viunga vya mji wa Zamalek polisi wa Misri waliizingira nyumba yake na watu walioshuhudia wanasema kulikuwa na ufyatulianaji wa riasasi kabla ya yeye kuamua kujisalimisha.

Bwana al-Dam aliviambia vyombo vya habari vya kigeni kwamba walinzi wake walikabiliana na polisi wa Misri kwa sababu hawakufahamu ni akina nani. Haifahamiki kama kuna yeyote aliyejeruhiwa katika kisa hicho.

Baadae picha zilisambazwa zikimuonyesha Bwana al-Dam akiwa ndani ya gari ana tabasamu.

Jamaa huyo wa Hayati Muammar Gaddafi aliwapungia watu mkono na alisikika akisema kwamba alikuwa amehiari yeye mwenyewe kwenda kwa Mkuu wa polisi kulalamika.

Katika siku za hivi majuzi serikali ya Libya imekuwa ikiishinikiza Misri kuwakabidhi raia kadhaa wa Libya wanaohusishwa na utawala wa Gaddafi.