ICC yampongeza Ntaganda kujisalimisha

Image caption Jenerali Bosco Ntaganda, kiongozi wa waasi Congo

Mahakama ya Kimataifa ya Kushughulikia Makosa ya Jinai, ICC, imempongeza kiongozi wa waasi, Bosco Ntaganda kwa kujisalimisha na kuwa tayari kukabiliana na mashitaka ya uhalifu wa kivita, katika mahakama hiyo.

Akijulikana kama "The Terminator", Jenerali Ntaganda alijisalimisha Jumatatu wiki hii katika ubalozi wa Marekani nchini Rwanda baada ya miaka saba ya kutafutwa na mahakama ya ICC.

ICC imesema imekuwa katika mawasiliano na mamlaka zinazohusika ili kumwezesha Jenerali Ntaganda kusafirishwa mara moja kwenda The Hague.

Amekanusha kuhusika na makosa ya utesaji, ubakaji na mauaji wakati wa mgogoro wa muda mrefu katika Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo.

Serikali ya Congo imesema Jenerali Ntaganda aliingia nchini Rwanda Jumamosi iliyopita kwa msaada wa majeshi ya Rwanda.

Rwanda imekuwa ikikanusha tuhuma dhidi yake kuwa imekuwa ikisaidia vikundi vya waasi dhidi ya serikali ya Jamhuri ya Congo.