Wazimbabwe waunga mkono Katiba Mpya

Image caption Rais wa Zimbabwe Robert Mugabe kulia na Waziri Mkuu Morgan Tsvangirai

Raia wa Zimbabwe wamepitisha mswada wa katiba mpya kwa wingi wa kura ya maoni iliyopigwa siku ya jumamosi, Tume ya Uchaguzi imesema.

Katiba hiyo mpya ambayo inaweka ukomo wa urais kwa mihula miwili ya miaka mitano mitano imeungwa mkono karibu na asilimia 95 ya wapiga kura.

Katiba hiyo pia imeungwa mkono na vyama viwili vikuu vya siasa nchini humo ambavyo vimeunda serikali ya umoja wa kitaifa tangu mwaka 2009.

Kupitishwa kwa katiba hiyo ni mwanzo wa safari ya kuelekea katika uchaguzi Mkuu wa nchi hiyo mapema mwaka huu.

Wakati huo huo shirika la kutetea haki za binadamu la Human Rights Watch limesema serikali inapaswa kuhakikisha polisi hawafanyi msako dhidi ya mashirika ya kiraia ambayo yamekuwa yakifuatilia masuala ya uchaguzi.

Katika kutekeleza katiba hiyo mpya ibara inayoweka ukomo wa urais haitazingatia mambo ya nyuma, hivyo kiongozi wa Zanu-PF rais wa sasa wa nchi hiyo Robert Mugabe ataruhusiwa kugombea urais wakati wa uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika mwezi July.

Rais Robert Mugabe anatarajiwa kupambana na kiongozi wa Movement for Democratic change (MDC) Morgan Tsvangirai ambaye kwa sasa ni Waziri Mkuu katika serikali ya umoja wa kitaifa.

Katika matokeo yaliyotangazwa na Tume ya Uchaguzi Wazimbabwe waliopiga kura ya "ndio" kuunga mkono katiba mpya walikuwa 3,079,966 huku 179,489 wakipiga kura ya "hapana" na kura 56,627 zikiharibika.