Al-Qaeda yadai kumuua Mfaransa

AQIM imechapisha picha za Bwana Verdon (kulia) na mwenzake
Image caption AQIM imechapisha picha za Bwana Verdon (kulia) na mwenzake

Kikundi cha Al-Qaeda Afrika Kaskazini (AQIM) kinasema kwamba kimemuua mfanyibiashara Mfaransa aliyetekwa nyara nchini Mali mnamo 2011, shirika la habari la Mauritania, ANI, limesema.

AQIM iliiambia ANI kwamba ilimuua Philippe Verdon mnamo Machi 10, ili kulipiza kisasi kuingia kwa majeshi ya Ufaransa nchini Mali.

Wanajeshi wa Ufaransa walitumwa nchini Mali Januari mwaka huu baada ya wanamgambo wa Al-Qaeda kuonya kwamba wangeuvamia mji mkuu, Bamako.

Hivi karibuni, majeshi yanayoongozwa na Ufaransa yamekuwa yakipigana dhidi ya wanamgambo hao katika milima ya Ifoghas, huko Mali kaskazini.

Mapema Jumatano, Wizara ya Mambo ya Nje ya Ufaransa ilikuwa inajaribu kuthibitisha ripoti hizo kutoka kwa ANI.

Bamako

Mbali na Bwana Verdon, jumla ya Wafaransa 14 wanazuiliwa na makundi ya Kiisilamu barani Afrika.

Kwa sasa Ufaransa ina wanajeshi 4,000 nchini Mali wanaoasaidiwa na maelfu ya wanajeshi kutoka Mali, Chad na nchini nyingine za Kiafrika.

Ufaransa iliingilia kati baada ya muungano wa wanamgambo wa Kiisilamu na waasi kuteka eneo la Mali kaskazini mwaka uliopita, na kutoa onyo kwamba walikuwa wananuia kuelekea Bamako.

Lakini tangu majeshi hayo yaingilie kati, maeneo kadhaa yameshasalimishwa, ingawaje mapigano yangali yanaendelea katika milima iliyopo jangwani.

Ufaransa inanuia kuondoa majeshi yake kutoka Mali mwezi ujao, huku nchi za Afrika Magharibi zikitegemewa kuziba pengo hilo. Uchaguzi unanuiwa kufanywa mnamo Julai.