Wanariadha wa Kenya watetewa kuhusu madawa

Wanariadha wafanya mazoezi
Image caption Wanariadha wafanya mazoezi

Wasimamizi wa michezo nchini Kenya wamekanusha habari kwamba wanariadha wengi hutumia madawa ya kuwaongezea nguvu.

Katibu-mkuu wa shirika la Athletics Kenya, David Okeyo, amesema visa vilivyoripotiwa vilikuwa vinahusiana na kutumika kwa dawa zilizotolewa na madaktari kutibu maradhi ya kawaida kama asthma na kikohozi.

Bwana Okeyo amesema kwamba kuna baadhi ya wanariadha waliomeza dawa hizo bila kujua kwamba zilikuwa zimepigwa marufuku na wanaosimamia spoti.

Mnamo Alhamisi, Athletics Kenya iliwapiga marufuku wanariadha wawili wanaokimbia mbio za marathon.

Idadi ya wanariadha waliopogiwa marufuku sasa imefikia watano kwa muda wa mwezi mmoja uliopita.

Juma lililopita, shirika linalosimamia riadha duniani, IAAF, lilisema kwamba litaweka maabara ya muda nchini Kenya litakalochunguza utumizi wa madawa yasiyokubalika.