Bangui yatekwa na wapiganaji

Wanajeshi wa Jamhuri ya Afrika ya Kati

Wapiganaji wa Jamhuri ya Afrika ya Kati wanasema kuwa wameiteka ikulu katika mji mkuu, Bangui.

Rais Francois Bozize hajakuwapo ikulu wakati huo na wanasema amekimbilia nchi ya jirani ya Jamhuri ya Demokrasi ya Congo.

Msemaji wa rais alisema kuwa wapiganaji sasa wanadhibiti Bangui na anatumai hapatakuwa na vitendo vya kulipiza kisasi.

Risasi zinaendelea kusikika kwenye bara-bara za mjini Bangui.

Mwandishi wa habari wa shirika la Ufaransa mjini humo anasema Jumapili alfajiri risasi nyingi zilisikika karibu na ikulu ya rais, na milio ya risasi ni ya hapa na pale.

Rais Francois Bozize mwenyewe alinyakua madaraka kwenye mapinduzi miaka 10 iliyopita; na tangu wakati huo amekuwa akijaribu kuiweka nchi pamoja kukiwa na mashindano na mapigano kati ya makabila na koo.

Msemaji wa kundi la wapiganaji la Seleka - ambalo lenyewe ni ushirikiano wa makundi matatu - ameliambia shirika la habari la Ufaransa kwamba wanawaomba wafuasi wao wasiibe ngawira au kulipiza kisasi dhidi ya watu wa jiji.

Ufaransa, ambayo ilwahi kuitawala nchi hiyo, ina wananchi wake zaidi ya 1000 mjini Bangui na kikosi kidogo.

Imewashauri wananchi wake wabaki majumbani mwao.

Wapiganaji walianza mashambulio yao mwezi Disemba lakini walijizuwia kushambulia mji mkuu.

Wapiganaji walifikia makubaliano na serikali mwezi wa Januari lakini yalivunjika wiki chache zilizopita, kwa sababu wapiganaji wanasema, serikali ilikataa kuwaachilia huru wafungwa wa kisiasa na haikutimiza shuruti zao.