Ufaransa yawaonya waasi wa CAR

Waasi wa Seleka
Image caption Waasi wa Seleka

Ufaransa imewaomba viongozi wa waasi nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati, CAR, waheshimu haki za bindamu. Waasi hao walivamia mji mkuu, Bangui, na kuipindua serikali.

Rais wa Ufaransa Francois Hollande, ambaye ameshatuma mamia ya wanajeshi huko, amesema kwamba waasi hao yafaa wawaheshimu wananachi.

Bwana Hollande alithibitisha kwamba Rais Francois Bozize ameshatoroka CAR. Yaaminika kwamba yuko mjini Zongo, DRCongo.

Waasi wamekuwa wakimshurutisha Bozize ajiuzulu, wakisema kwamba amevunja mikataba kadhaa kati yao na serikali yake.

Mapigano

Walianza kupigana Desemba mwaka uliopita, na baada ya mapigano ya majuma kadhaa wakakubali kujiunga na serikali ya mseto.

Lakini mapigano yalizuka tena wiki iliyopita, baada ya waasi kudai wafungwa wa kisiasa waachiliwe huru.

Waliuteka mji mkuu haraka, na Bwana Bozize alitoroka mapema Jumapili.

Nelson Ndjadder, msemaji wa mmojawapo ya makundi wanachama wa Seleka, amesema sasa CAR inawezachukua kupiga hatua mbele iwapo uchaguzi wa kidemokrasia utaweza kufanyika.

Majadiliano

"Kwa vile tumeuteka mji wa Bangui na Bozize kaondoka, kusudi letu limeshatimia," alisema.

"Wananchi wa CAR sasa hawanabudi kuketi na kukutana ili kuamua hatima ya nchi hii."

Wauguzi mjini Bangui wanasema kuna hali ya utata mjini humo, na kwamba kazi yao inatatizwa na kukatika kwa umeme mara kwa mara.

Shirika la Msalaba Mwekundu limesema kwamba mahospitali yanawapokea majeruhi wengi wa mapigano.

Uporaji

Amy Martin wa shirika la kutoa misaada la Umoja wa Mataifa, OCHA, aliiambia BBC kwamba maeneo mengi yameporwa.

"Hali haieleweki... tunaafiriwa kwamba hata hospitali ya watoto imeporwa," alisema.

Walindaamani wa Afrika Kusini waliokuwepo CAR ili kulisaidia jeshi la serikali nao walijeruhiwa. Walishindwa kuwazuia waasi hao.

Bi Martin anasema kwamba walindaamani sasa wanapanga kuondoka nchini humo.

Umaskini

CAR, yenye takriban wakaazi milioni 4.5, imekumbwa na uasi mara kadhaa tangu uhuru toka Ufaransa mnamo 1960.

Ni mmojawapo wa nchi maskini barani Afrika, ingawaje ina utajiri mkubwa wa madini.