Nelson Mandela hospitalini tena

Image caption Nelson Mandela alikuwa rais wa kwanza mweusi wa Afrika Kusini

Rais wa zamani wa Afrika Kusini, Nelson Mandela amelazwa tena hospitalini baada ya kuugua ugonjwa wa mapafu kwa mara nyingine.

Taarifa kutoka kwa serikali ya nchi hiyo, ilisema kuwa Mandela mwenye umri wa miaka 94 alilazwa hospitalini muda mfupi kabla ya saa sita usiku.

Mandela alilazwa siku kumi na nane hospitalini mwezi Disemba mwaka jana kupokea matibabu ya ugonjwa wa mapafu na kibofu.

Anasifika sana kama baba wa taifa hilo kwa kuongoza vita dhidi ya utawala wa ubaguzi wa rangi.

Kadhalika Mandela alihudumu kama rais wa kwanza mweusi Afrika Kusini tangu mwaka 1994 hadi mwaka 1999, ingawa hali yake ya kiafya imezua wasiwasi kwa muda sasa.

Rais Jacob Zuma alimtumia taarifa ya kumpa pole na kumtakia kupona Mandela

"tunawataka watu wa Afrika Kusini pamoja na duniani kote kuwa watulivu na kumuombea Madiba na familia yake. Tuna imani kuwa kikosi cha madaktari wanaomtibu Mandela watafanya kila hali kuhakikisha anapona,'' alisema Zuma katika taarifa yake.

Mapema mwezi huu bwana Mandela alilazwa hospitalini mjini Pretoria baada ya kufanyiwa ukaguzi wa kiafya.