Usalama wadhibitiwa Kenya

Image caption Polisi wa kupambana na ghasia wako tayari kukabiliana na wale watakaozua ghasia

Polisi wamedhibiti usalama kote nchini Kenya huku uamuzi wa mahakama ya juu zaidi kuhusu kesi inayopinga ushindi wa rais mteule Uhuru Kenyatta katika uchaguzi uliofanyika Machi nne.

Aidha majaji wanatarajiwa kutoa uamuzi wao katika saa chache zijazo.

Barabara zote kuelekea katika mahakama ya juu zimefungwa.

Kikosi cha polisi wa kupambana na ghasia GSU, polisi wa utawala wa mikoa na wale wa kawaida, wameziba makutano ya barabara za Wabera na Mama Ngina, City Hall Way, majengo ya bunge na barabara za Taifa.

Hata hivyo wafanya biashara katika soko maarufu linalouza bidhaa zinazotengezwa na wamasai, wameruhusiwa kuuza bidhaa zao.

Afisaa mkuu wa polisi Moses Ombati alitembelea soko hilo asubihi na mapema na kuwahakikishia wafanyabiashara usalama wao.

Alionya kuwa maafisa wa polisi wamepelekwa katika soko hilo kukabiliana na wale wanaohujumu hali na kuchochea ghasia.

Siku ya Ijumaa, mkuu wa polisi David Kimaiyo aliahidi kukabiliana vilivyo na vitendo vyovyote haramu huku uamuzi wa mahakama ukisubiriwa.

Makundi yameanza kukusanyika mjini kusubiri uamuzi huo wa kihistoria.

Mahakama hiyo itaamua kesi ya kihistoria ambayo watatoa uamuzi ikiwa Uhuru Kenyatta ataapishwa kama rais au kama uchaguzi utarejelewa kati ya wagombea wa urais Kenyatta na waziri mkuu Raila Odinga.