Mpiganaji auwawa Timbuktu

Wakuu wa jeshi nchini Mali wanasema mshambuliaji aliyejitolea mhanga ameuwawa, akijaribu kujiripua kwenye kituo cha ukaguzi mjini Timbuktu, kaskazini mwa nchi.

Mwanajeshi mmoja alijeruhiwa.

Mwandishi wa BBC nchini Mali anasema tangu wakati huo risasi zimekuwa zikifyatuliwa magharibi mwa mji huo.

Timbuktu imekuwa mikononi mwa wapiganaji wa Kiislamu kwa miezi kumi hadi walipofurushwa na wanajeshi wa Ufaransa awali mwezi March.

Wanajeshi wa Ufaransa na Afrika wanasema wamefanikiwa kuzuwia uvamizi wa eneo la kaskazini mwa Mali uliofanywa na wapiganaji wa Kiislamu.

Ufaransa itaanza kuondosha wanajeshi wake mwezi Aprili lakini baadhi yao watabaki, pengine watajumuika na kikosi cha Umoja wa Mataifa.