Wanamgambo washambulia Kituo cha umeme Pakistan

Wapiganaji nchini Pakistan wamefanya shambulio la kombora katika kituo kimoja cha umeme kwenye mji wa kaskazini wa Peshawar.

Takriban watu watano waliuwawa na maafisa kadhaa wa Polisi kujeruhiwa. Wapiganaji hao walivamia kituo hicho gizani.

Polisi wanasema watu wawili waliuwawa papo hapo kabla ya wavamizi kutoroka huku wakiwachukua mateka kumi.

Wengine watano waliuwawa karibu na eneo hilo.

Waliofariki walijumuisha maafisa wa polisi na wafanyikazi wa kituo cha umeme.

Hadi kufikia sasa waliotekwa nyara hawajulikani waliko na msako unaoongozwa na maafisa wa usalama, unaendelea.

Kundi la Taliban nchini Pakistan ambalo hutekeleza mashambulio ya mara kwa mara Kaskazini Magharibi, halijakiri kuhusika na shambulio hilo.

Kumekuwa na wasiwasi kuwa wapiganaji hao huenda wakaimarisha mashambulio yao kabla ya uchaguzi mkuu wa mwezi Mei.