Kashfa za kuwaharibu watoto kuchunguzwa Australia

Image caption Bi Julia Gillard amesema ukweli utadhihirika

Tume ya kitaifa inatarajiwa kuanza kuchunguza kashfa za udhahlilishaji wa watoto kingono mjini Melbourne, Australia.

Zaidi ya watu 5,000 wanatarajiwa kutoa ushahidi wa dhulma hizo na kuelezea athari walizopata.

Waziri mkuu Julia Gillard, ameonya kuwa tume hiyo itaweza kuibuka na ukweli ambao kwa baadhi ya watu huenda ikawa kero kubwa.

Alisema kuwa ufunguzi rasmi wa tume hiyo ni hatua muhimu ya kimaadili kwa Australia.

Tume hiyo itachunguza makundi ya kidini , asasi za kijamii na wahudumu wa afya wa serikali,pamoja na mashirika mengine ya serikali.

Lakini maafisa wa tume hiyo wameonya kuwa huenda wasikamilishe kazi yao ifikapo mwaka 2015 kama wanavyotakiwa.

Walisema kuwa ni kwa sababu ya wingi wa kesi walizopokea, ikilinganishwa na idadi ya watu wanaotarajiwa kutoa ushahidi wao na idadi ya tasisi zilizoshtumiwa.

Uchunguzi utaangalia majibu ya taasisi zilizoshutumiwa kuhusika na kuwaharibu watoto au kuwadhalilisha kingono.

Kuundwa kwa tume hiyo, kulitangazwa na waziri mkuu Bi Gillard mwezi Novemba kufuatia shinikizo kutoka kwa wabunge baada ya madai ya polisi kuwa kanisa katoliki lilifutilia mbali ushahidi wa makasisi waliowaharibu watoto.

Bi Gillard alisema kuwa anataka tume hiyo kutoa uponyo kwa waathiriwa wa vitendo hivyo, kwa sababu kwa muda mrefu wengi wa waathiriwa hawajapata msaada

Visa vya kuwaharibu watoto, vinavyofanywa na makasisi vimekuwa swala tete nchini Australia katika miaka ya hivi karibuni.

Mwezi Septemba, kanisa katoliki katika jimbo la Victoria walithibitisha kuwa zaidi ya watoto miasita waliharibiwa na makasisi tangu mapema miaka ya thelathini.

Wakati wa ziara yake nchini Australia mwaka 2008, Papa mstaafu Benedict, alikutana na baadhi ya waathiriwa na koumba msahama hadharani.