Msako wa Kony wasitishwa Afrika ya Kati

Image caption Mtoro Joseph Kony

Serikali ya Uganda inasema kuwa imesitisha msako wake wa kiongozi mtoro wa waasi wa LRA Joseph Kony, katika Jamuhuri ya Afrika ya Kati.

Uganda inasema imeamua kuchukua hatua hiyo kufuatia mgogoro wa kisiasa unaokumba taifa hilo baada ya rais Francois Bozize kung'olewa mamlakani.

Pia imeelezea kuwa serikali ya mpito inayoongozwa na kiongozi wa waasi imetatiza shughuli zao.

Uganda inasema kuwa wanajeshi wake katika eneo hilo ambako waasi walichukua mamlaka siku kumi zilizopita, watasalia katika kambi zao hadi muungano wa Afrika utakapotoa mwongozo.

Joseph Kony anayeongoza kundi la waasi wa LRA, anatakikana na mahakama ya kimataifa ya jinai kwa tuhuma za uhalifu wa kivita.

Anaaminika kujificha na wapiganaji wake katika misitu inayopakana na Jamuhuri ya Afrika ya Kati, Sudan Kusini na Jamuhuri ya kidemokrasia ya Congo.