Upara,sababu ya maradhi ya moyo?

Wanaume wanaoanza kuwa na upara huenda wakakabiliwa zaidi na tisho la maradhi ya moyo kuliko wenzao waliojaa nywele vichwani.

Hii ni kwa mujibu wa watafiti nchini Japan.

Utafiti huu uliowahusisha watu 37,000, ulichapisha taarifa kwenye jarida la mtandao, 'BMJ Open' ukisema kuwa wanaume wanaokuwa na upara kwa asilimia 32 wanaweza kuwa na maradhi ya moyo.

Hata hivyo, watatifi walisisitiza kuwa athari hizi ni chache ikilinganishwa na zile za uvutaji sigara na unene kupita kiasi.

Shirika linalojikita katika maswala ya maradhi ya moyo nchini Uingereza, limesema kuwa wanaume wanapswa kujichunga wasinenepe kupita kiasi kuliko kuchunga nywele zao.

Kuanza kukuwa na kipara ni kawaida ya maisha kwa wanaume . Wengi kuanza kukuwa na upara wanapokuwa miaka 50 na asilimia 80 ya wanaume hao, hupoteza nywele wanapokuwa na umri wa miaka 70.

Watafiti katika chuo kikuu cha Tokyo, walidurusu utafiti wa miaka mingi iliyopita, kuchunguza uhusiano uliopo kati ya kuwa na upara na maradhi ya moyo.

Walionyesha kuwa nywele ambazo zilianza kutoweka, zina uhusiano na maradhi ya moyo. Hii ilikuwa baada ya kuzingatia maswala kama umri, na historia ya familia.

Daktari, Tomohide Yamada, wa chuo kikuu cha Tokyo alisema kuwa walipata uhusiano mkubwa kati ya upara na tisho la kupata maradhi ya moyo.

"tuliona hili kama jambo muhimu, lakini halina athari kubwa kama mambo mengine yanayosababisha maradhi ya moyo kama vile uvutaji sigara, unene kupita kiasi na mafuta mengi mwilini pamoja na shinikizo la damu.''

Alisema kuwa wanaume wenye umri mdogo wanaopata upara wanapaswa kuanza kuzingatia afya njema ili kujikinga kutokana na maradhi ya moyo

Aidha alisema hakuna ushahidi wa kutosha kupendekeza kuwa wanaume wenye upara wafanyiwe uchunguzi wa maradhi ya moyo.

Maradhi ya moyo ndio moja ya sababu kuu za vifo nchini Uingereza.

Mmoja kati yawanawake wanane kufariki kutokana na maradhi ya moyo.

Husababishwa na mishipa ya damu ambayo husukuma damu kwa moyo pale inapoziba.

Mmoja wa madaktari wakuu Uingereza amesema kuwa ingawa utafiti huu unaibua hisia, wanaume wenye upara hawapaswi kuwa na hofu.