Saudia yapata hasara kufukuza wageni

Hatua ya serikali ya Saudi Arabia ya kuwafukuza wageni wasiokuwa na kibali inaendelea kusababisha maduka, biashara na shule kufungwa.

Wafanya biashara katika bandari ya mji wa Jeddah wameviambia vyombo vya habari kwamba vyakula vimeanza kuoza kwa sababu asili-mia-20 tu ya makuli wanakwenda kazini.

Kufuatana na sheria mpya za ajira za Saudi Arabia kanuni za kuleta wageni zimekuwa kali, na maelfu ya wafanyakazi wasiokuwa na ruhusa wamekamatwa na watarejeshwa makwao.

Lengo ni kufanya nchi ipunguze kutegemea wageni na nafasi za kazi wapewe Wasaudi wenyewe.